30 Desemba 2021 - 10:44
Hamad bin Jassim: Maafikiano tarajiwa ya madola Magharibi na Iran ni fursa ya kupunguza mizozo

Waziri Mkuu wa zamani wa Qatar amezungumzia mwenendo wa mazungumzo ya nyuklia ya Iran na kundi la 4+1 yanayoendelea huko Vienna Austria na kueleza kwamba, maafikiano tarajiwa baina ya madola Magharibi na Iran ni fursa ya kupunguza mizozo katika eneo la Asia Magharibi.

Shirika la habari la Ahlubayt (as)ABNA: Hamad bin Jassim amesisitiza kuwa, hatua yoyote ile ya moja kwa moja ya kijeshi dhidi ya mataifa ya eneo itakuwa na taathira hasi.

Waziri Mkuu wa zamani Qatar aidha ameongeza kuwa, hatua ya kijeshi dhidi ya mataifa ya Asia Magharibi kwa hakika haiwezi kudhamini maslahi yetu si kwa muda mfupi wala muda mrefu.

Hivi karibuni pia Hamad bin Jassim alinukuliwa akisema kuwa, Iran na madola ya Magharibi zitafikia makubaliano, hivyo ni vyema mataifa ya Ghuba ya Uajemi yakafanya mazungumzo na Iran.

Duru ya nane ya mazungumzo ya Vienna yanayoangazia suala la kuondolewa vikwazo vya kidhalimu na haramu dhidi ya Iran ilianza Jumatatu iliyopita kwa kikao cha Kamisheni ya Pamoja iliyoongozwa na Ali Bagheri, mkuu wa timu ya mazungumzo ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Enrique Mora, ambaye ni Naibu Katibu Mkuu wa Huduma ya Kigeni ya Umoja wa Ulaya.

Akizungumza jana, Hussein Amir-Abdollahian, Waziri wa Mashauri ya Kigeni ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran alieleza matumaini yake ya kufikiwa mapatano ya kuridhisha katika mazungumzo ya nyuklia ya Iran na kundi la 4+1 linaloundwa na mataifa ya Russia, China, Uingereza, Ufaransa pamoja Ujerumani yanayoendelea huko Vienna, Austria.

342/